1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yachunguza kifo cha mfanyakazi wake Rafah

Angela Mdungu
15 Mei 2024

Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi wa shambulio lililolenga gari la Umoja wa Mataifa na kumuua mfanyakazi wake wa kwanza wa kimataifa katika ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7.

https://p.dw.com/p/4fsG3
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa Rafah
Wapalestina wakiomboleza kando ya mwili wa afisa wa UN aliyeuwawa mjini RafahPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Umoja wa Mataifa amesema kuwa uchunguzi huo umeanzishwa ili kubaini ukweli wa shambulio lililomuuwa mfanyakazi wake Jumatatu wiki hii. Mfanyakazi huyo aliyekuwa afisa mstaafu wa jeshi la India Waibhav Anil Kale, alikuwa mfanyakazi wa idara ya ulinzi na usalama ya Umoja wa mataifa.

Alikuwa njiani ndani ya gari kuelekea katika hospitali ya Ulaya ya mjini Rafah pamoja na mwenzake aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Kutokana na tukio hilo, wizara ya mambo ya kigeni ya India imesema Jumatano kuwa, ujumbe wake wa kidiplomasia unawasiliana na mamlaka husika kuhusu uchunguzi huo na katika kusaidia kurejesha nyumbani mabaki ya mwili wa afisa huyo aliyeuwawa.

Wapalestina wafanya maadhimisho ya miaka 76 ya Nakba

Katika hatua nyingine, Wapalestina kote Mashariki ya kati wanaadhimisha miaka 76 tangu wengi wao walipofuzwa kutoka eneo linalofahamika sasa kama Israeli. Maadhimisho hayo yanafanyika kwa maandamano na matukio mengine Mashariki ya kati wakati kukiwa na wasiwasi mkubwa juu ya janga la kiutu linaloendelea Gaza.

Soma zaidi: Nakba - "maafa" ya Wapalestina

Wakati wa Nakba, neno la kiarabu linalomaanisha 'janga',  takriban Wapalestina 700,000, walikimbia au walifukuzwa kutoka makwao kabla na wakati wa vita vya Waarabu na Israeli vya mwaka wa 1948 na kusababisha kuanzishwa kwa nchi ya Israeli.

Palestina inaadhimisha miaka 76 ya Nakba
Wakimbizi wa Kipalestina wakati wa Nakba mwaka 1948Picha: ELDAN DAVID/EPA/dpa/picture-alliance

Wakati huohuo, Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umewaambia wabunge wa nchi hiyo kuwa utaipatia Israel msaada wa ziada wa silaha wa zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 1. Hata hivyo haikubainishwa ni lini hasa silaha hizo zitapelekwa Israel. Huu ni msaada wa kwanza wa silaha kwa Israeli kuwekwa wazi  tangu utawala wa Biden ulipozuia silaha nyingine nchini humo ambazo ni pamoja na mabomu 3,500 mapema mwezi huu.